Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kwa kunukuu tovuti ya Mir’at al-Bahrain, Latifa Al-Husseini, mwandishi na mwanahabari wa Lebanon, katika makala yenye anuani “Pamoja na Mateso ya Kila Siku ya Wabahrain”, aliandika:
Katika kilele cha hali ya sasa ya Bahrain iliyojaa migogoro, ukandamizaji na mashaka makubwa, nilimuuliza mmoja wa raia wa Bahrain: “Ni lipi gumu zaidi kwako; kunyang’anywa uraia au kufungwa jela kwa muda mrefu ndani ya nchi yako?” Sikupata jibu la moja kwa moja; huenda kwa sababu chaguo zote mbili ni za kikatili, pia nilimsikia raia mwingine akisema: “Watu wetu leo aidha wako gerezani, au wamekuwa wahamaji wasio na uraia, au wamekuwa mashahidi!”
Aliongeza: Nchini Bahrain, ili kuhisi maumivu na mapigo ya moyo ya wananchi, si lazima uwe na uraia wa nchi hiyo au uwe raia wa asili, wote wako chini ya uangalizi, vitisho, ufuatiliaji, mzingiro na vikwazo, na hatimaye wote wako katika mstari wa kulengwa. Hawakumbuki kamwe hali ya kubanwa na kunyimwa uhuru kama wanayoipitia leo; nchi ambayo inasisitiza hata kudhibiti fikra na itikadi zao.
Al-Husseini aliendelea: Hali hii ngumu inaonekana wazi katika maisha ya kila siku ya watu, kila mmoja anakabiliwa na aina ya ugaidi wa kudumu; vyombo vya usalama vinavizia ili kumwangukia kila raia ambaye huonekana kuwa “kero” kwa serikali. Huenda Bahrain ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya wananchi wanaoitwa mara kwa mara na kuulizwa: “Kwa nini uliandika jambo hilo? Kwa nini ulisema hili? Na kwa nini uliikosoa mada hiyo?”
Mwandishi huyo wa Lebanon alisema: Leo hii, mazungumzo kuhusu kuongeza adhabu husikika nchini Bahrain pekee, kuzungumzia kifungo cha maisha au kunyimwa uraia kwa uwazi kabisa husikika nchini Bahrain pekee, shughuli kubwa za taasisi rasmi katika uwanja wa makosa ya mtandao husikika nchini Bahrain pekee, hali ya utiifu kamili kwa mtawala pamoja na kumtukuza na kumheshimisha kupita kiasi ni jambo linaloonekana nchini Bahrain pekee, rangi moja katika vyombo vya habari na vichwa vya habari vilivyonakiliwa kwa mtindo mmoja katika magazeti ni jambo linaloonekana nchini Bahrain pekee, kunyang’anywa utambulisho wa kitaifa wenye mizizi ya mamia ya miaka ni jambo linalotokea nchini Bahrain pekee.
Aliashiria: Haya yote ni kwa ajili ya nini? Ni kwa sababu tu sehemu kubwa ya wananchi wamechagua kushikamana na itikadi zao za Kiislamu; itikadi ambazo leo zimekuwa “mstari mwekundu” kwa dola ya kipolisi, kundi ambalo kwa ikhlasi na uthabiti wake katika kushikamana na Wilayah, mafundisho ya Ahlul-Bayt (as) na shule ya Imam Hussein (as), limeweza kuvutia umakini wa Waislamu wote Waarabu, hususan wafuasi wa madhehebu ya Ithna Ashariyyah, na kuwa mfano wa kweli wa imani ya kimaumbile kwa dini halisi ya Muhammad (s.a.w.w.) na mfano hai wa “Jihadi ya Ufafanuzi” katika zama za watawala madhalimu.
Al-Husseini aliendelea: Leo, taifa zima linaishi katika hali ya msongo wa mawazo wa kudumu, watu hawaogopi tu kukamatwa, bali pia wanaogopa kuongezwa katika orodha mpya za hukumu nzito za mahakama au kuona majina yao yakitajwa katika habari za uvamizi na kesi za haraka kwa tuhuma ambazo hata hazistahili kuitwa tuhuma, kila siku mduara wa wasiwasi unazidi kupanuka, na raia anajihisi amezingirwa kati ya ukimya unaomuumiza na neno ambalo linaweza kumgharimu maisha ya kufuatiliwa na kusakwa.
Mwandishi huyo wa habari alisisitiza: Katika miji na vijiji kuna nyuso ambazo huzuni zimezibadilisha taratibu; mama anayesubiri simu kutoka kwa mwanawe aliyekamatwa, baba anayeficha machozi yake ili familia isisambaratike, na watoto wanaokua huku wakiwa na picha za wapendwa wao walioko nyuma ya nondo za magereza.
Hizi si simulizi za mtu mmoja mmoja tu, bali ni taswira ya pamoja ya taifa linaloteseka kimya kimya.
Alisema: Kinachoumiza zaidi kuliko kukamatwa ni hisia ya jumla inayompata kila anayefuatilia habari za Bahrain; kwamba haki si tena mahali salama pa kukimbilia kwa wananchi, pale hukumu zinapokuwa za kutisha kwa ukali wake, raia hujihisi amevuliwa kinga mbele ya hofu, na huona kwamba hatima yake inaweza kubadilika kwa sababu ya neno moja, msimamo mmoja, au hata “shaka” moja tu, na katika mazingira kama hayo, jamii hupoteza hisia ya usalama.
Al-Husseini aliongeza: Inasemekana kwamba mataifa hayadumu kwa hofu wala kwa misako isiyo na mipaka, bali hudumu kwa haki ambayo wananchi wanaihisi kuwa ya uadilifu; kwa mazingira yanayomruhusu raia kupumua bila kuogopa kesho yake, hii ndiyo picha na hali halisi ya Bahrain ya leo; wasiwasi wa kiusalama ni jambo la kudumu, na serikali daima inatekeleza miradi ya “kusafisha” nchi dhidi ya wale inaowaita “wafuasi wa Wilayat al-Faqih”.
Mwandishi huyo wa Lebanon alihitimisha kwa kusema: Bahrain inahitaji uvumilivu na ustahamilivu, si ukatili; inahitaji wakati wa haki na insafu ili kuponya uchovu uliokusanyika katika nyoyo za watu wake, inahitaji wananchi wahisi kwamba wao ni raia wa daraja la kwanza, si kwamba wamezingirwa na watu wenye misimamo ya kimadhehebu wanaowachukia, wala wasiwe daima chini ya kivuli cha tuhuma, mataifa yanaweza kuvumilia matatizo kwa muda mrefu, lakini hayatakaa yasahau hisia ya kuachwa peke yao na kukata tamaa pale ambapo hofu inageuzwa kuwa “mtindo wa maisha”.
Maoni yako